Huku vitendo vya mabavu vikiendelea
dhidi ya wapinzani wanaopinga hatua ya rais wa Burundi kugombea tena
nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu ujao, Umoja wa Afrika ulitangaza siku
ya Jumapili kuwa umetuma nchini humo ujumbe wa ngazi za juu kwa ajili ya
kutafuta njia ya kutatua kwa amani mgogoro unaoikumba nchi hiyo. Ujumbe
huo unaoongozwa na Bwana Edem Kodjo, Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa
Nchi huru za Afrika OAU utafanya mazungumzo na viongozi wa serikali ya
Burundi, vyama vya siasa, wawakilishi wa mashirika ya kiraia na jamii ya
kimataifa na vilevile viongozi wa kidini ili kusuluhisha mgogoro huo.
Siku ya Jumamosi Umoja wa Afrika pia ulitoa taarifa ukisisitiza juu ya
udharura wa kufanyika mazungumzo kati ya pande zinazozozana ili kuandaa
mazingira ya kutatuliwa kwa amani mgogoro wa Burundi. Kabla ya hapo
umoja huo ulikuwa umetangaza kuwa mazingira ya Burundi hayaruhusu
kufanyika uchaguzi mkuu nchini humo. Hii ni katika hali ambayo Baraza la
Usalama wa Taifa la Burundi lilitoa taarifa hapo siku ya Jumamosi
likiwataka wapinzani na waandamanaji kusimamisha bila masharti yoyote,
maandamano yao ambayo yamevuruga maisha ya wananchi. Inaonekana kuwa
takwa hilo huenda likawakasirisha zaidi wapinzani wanaopinga hatua ya
Rais Pierre Nkurunziza ya kuwania tena kiti cha rais na hivyo kuzidisha
mvutano kati yao na askari usalama. Tayari mashirika ya kiraia yameitaja
amri hiyo kuwa ni tangazo la vita dhidi ya wananchi wa Burundi.
Yamesema hakuna rais wa nchi yoyote ile aliyeweza kushinda vita dhidi ya
taifa na kumtaka Rais Nkurunziza alitambue vyema suala hilo.
Licha
ya kuwa Burundi imekuwa ikishuhudia vitendo vya ghasia na machafuko kwa
miezi kadhaa sasa, lakini machafuko hayo yameongezeka kufuatia uamuzi wa
Rais Nkurunziza wa kuwania kwa mara ya tatu mfululizo, nafasi ya urais
na uamuzi huo kuungwa mkono na Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Wakati huohuo
serikali imeimarisha hatua za usalama na kutumia nguvui za jeshi dhidi
ya wapinzani. Kufikia sasa makumi ya watu wameuawa na kujeruhiwa katika
ghasia zinazoendelea huko Burundi ambapo Warundi wapatao 50,000
wamekimbilia usalama katika nchi jirani, jambo ambalo limeitia wasiwasi
mkubwa jamii ya kimataifa. Siku chache zilizopita nchi 15 wananchama wa
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mara nyingine zilitaka
kurudishwa utulivu nchini Burundi ili kuandaa mazingira ya kufanyika
uchaguzi huru na wa haki nchini. Wakati huohuo Jumuiya ya Nchi za Afrika
Mashariki imeandaa kikao huko Dar es Salaam mji mkuu wa Tanzania kwa
lengo la kutafuta njia za kutatua mgogoro wa Burundi. Wapinzani wa
Burundi wanasema kuwa hatua ya Rais Nkurunziza ya kugombea tena uchaguzi
inakinzana wazi na katiba ya nchi hiyo pamoja na makubaliano ya Arusha.
Licha ya kuwepo ghasia na machafuko nchini Burundi, lakini uchaguzi
mkuu unatarajiwa kufanyika kama ilivyopangwa, jambo ambalo wapinzani
wanasema hawataruhusu litimie, iwapo Rais Nkurunziza ataendelea
kushikilia msimamo wake wa kushiriki kwenye uchaguzi huo kinyume cha
sheria na katiba ya nchi.