manyaki-1.jpg ...      ...

Ajira za walimu hadharani

SERIKALI imetenga Sh bilioni tisa kwa ajili ya posho ya kujikimu na nauli kwa ajili ya walimu 31,056 na mafundi sanifu maabara 10,625, ambao ajira zao zimetangazwa jana huku wakitakiwa kuanza kazi Mei Mosi mwaka huu.
Aidha, watumishi hao wapya, wamehadharishwa juu ya ucheleweshaji, wakiambiwa kwamba, atakayeripoti mwisho wa mwezi wa Mei, hatapokewa isipokuwa, kama ana matatizo yanayotambulika.
Wakati kawaida walimu wapya hupangiwa halmashauri ambazo ndizo zenye jukumu la kuwapangia vituo vya kazi, kwa upande wa walimu wa sekondari wa masomo ya Sayansi na Hisabati ambao idadi yao ni 2,700, wamepangwa moja kwa moja kwenye shule ambazo hazina walimu.
Hayo yalibainishwa jana na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Jumanne Sagini alipokuwa akielezea kile alichosema ni sababu za kiufundi za kushindwa kutangaza majina ya ajira mpya za walimu Aprili 24, mwaka huu kama ilivyokuwa imetangazwa awali.
Katika kuhakikisha kunakuwa na uwiano sawa wa walimu na wanafunzi, halmashauri zilizojitosheleza au zenye idadi ya kuridhisha ya watumishi hao, hususani za mjini, hazikupangiwa kabisa walimu.
Posho Alisema fedha hizo ambazo ni posho ya kujikimu kwa siku saba na fedha za nauli zinatakiwa kulipwa na halmashauri ambao ni mwajiri. Zinatakiwa kulipwa ndani ya siku saba bila kuzidi siku 14 tangu kuripoti kwa mtumishi katika kituo cha kazi.
“Mwenye jukumu la kutuma fedha kwenye halmashauri ni Wizara ya Fedha. Lakini tumeziambia halmashauri zihakikishe zinalipa walimu ndani ya siku 14 tangu kuripoti na tuna uhakika kwamba halmashauri zina fedha,” alisema.
Alisema upo mfumo katika Tamisemi, ambao unaangalia fedha zilizoko katika halmashauri jambo alilosisitiza kwamba wanao uhakika kwamba zipo kuwezesha malipo hayo.
Akizungumzia haki za waajiriwa wapya, Sagini alisema mbali na posho za kujikimu, watarejeshewa fedha za nauli kwa njia ya basi au daraja la kawaida kwa usafiri wa treni.
Watatakiwa kujiunga katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii anaoupenda bila kupata ushawishi usio wa kawaida kutoka kwa mwajiri au mfumo.
Wachelewaji kutopokewa Aidha, Sagini alisema katika kuepuka watumishi wapya kukosa mshahara wa mwezi wa kwanza baada ya kuajiriwa, watumishi hao wametakiwa kuripoti kituo cha kazi kabla ya Mei 9, na kwamba kinyume chake, mtumishi huyo atalazimika kusubiri mwezi unaofuata alipwe na malimbikizo ya mshahara wa kwanza.
“ Kutokana na kuwapo watumishi wapya, Utumishi itaandaa mishahara kuanzia Mei 10, kwa maana hiyo mtumishi akichelewa kuripoti, hataweza kuingizwa katika orodha ya watu wanaotakiwa kulipwa na kama atafika mwisho wa mwezi wa Mei, hatapokewa, labda kama mtu huyo atakuwa na matatizo,” alisema na kuwataka kuripoti wakiwa na nyaraka zinazotakiwa.
Walimu wa sayansi Kuhusu walimu waliopangiwa vituo vya kazi moja kwa moja, alisema, “walimu wa masomo ya Sayansi waliohitimu ni wachache kuliko wa masomo ya Sanaa, hivyo tumeamua kuwapangia moja kwa moja vituo ili kuhakikisha kila shule inakuwa na walimu wa Fizikia, Kemia, Bayolojia na Hisabati.”
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo, serikali imeajiri walimu 11,795 wa cheti, 6,596 wa Stashahada, 12,666 wa Shahada na Mafundi Sanifu Maabara 10,625. Uwiano sawa Sagini alisema ajira za walimu kwa mwaka huu zimeelekezwa zaidi katika halmashauri zenye uhaba mkubwa wa walimu kuweka uwiano sawa na bora wa mwalimu na mwanafunzi kitaifa.
“Mfano Halmashauri ya Kaliua, Tabora iliyokuwa na uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 211, wamepelekwa walimu 1,143 ili kuwe na uwiano wa mwalimu 1:45 ambao ndio wastani unaoelekezwa na sera ya elimu,” alisema na kuongeza kuwa halmashauri zilizojitosheleza au zenye idadi ya kuridhisha hususani za mjini hazikupangiwa kabisa walimu.
Alitaja halmashauri ambazo hazikupangiwa walimu wapya ni Manispaa za Ilala, Temeke, Kinondoni, Dodoma, Singida, Songea, Tabora, Moshi na Halmashauri ya Mji Kahama.
Alihimiza halmashauri ambao ndio waajiri wa walimu, kupanga watumishi hao wapya kwa haki shule zote ziwe na walimu wa kutosha na kuweka utaratibu mzuri wa kuwapokea.
Kwa upande wa wahitimu ambao ni waajiriwa wa Serikali, alisema wanatakiwa kurudi kwa waajiri wao na kuendelea na kazi. “ Kuna baadhi ya walimu walioko kwenye ajira wakimaliza kujiendeleza na kuona wilaya aliyopo ina changamoto watajichomeka ili wapangiwe upya, wasifanye hivyo kwani wanapoteza haki zao kwani utumishi wataona ni kama mtu anataka ajira mara mbili,” alisema.http://frankmanyaki.blogspot.com/
Previous
Next Post »