manyaki-1.jpg ...      ...

Umoja wa Afrika na juhudi za kutatua kwa amani mgogoro wa Burundi

Huku vitendo vya mabavu vikiendelea dhidi ya wapinzani wanaopinga hatua ya rais wa Burundi kugombea tena nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu ujao, Umoja wa Afrika ulitangaza siku ya Jumapili kuwa umetuma nchini humo ujumbe wa ngazi za juu kwa ajili ya kutafuta njia ya kutatua kwa amani mgogoro unaoikumba nchi hiyo. Ujumbe huo unaoongozwa na Bwana Edem Kodjo, Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Nchi huru za Afrika OAU utafanya mazungumzo na viongozi wa serikali ya Burundi, vyama vya siasa, wawakilishi wa mashirika ya kiraia na jamii ya kimataifa na vilevile viongozi wa kidini ili kusuluhisha mgogoro huo. Siku ya Jumamosi Umoja wa Afrika pia ulitoa taarifa ukisisitiza juu ya udharura wa kufanyika mazungumzo kati ya pande zinazozozana ili kuandaa mazingira ya kutatuliwa kwa amani mgogoro wa Burundi. Kabla ya hapo umoja huo ulikuwa umetangaza kuwa mazingira ya Burundi hayaruhusu kufanyika uchaguzi mkuu nchini humo. Hii ni katika hali ambayo Baraza la Usalama wa Taifa la Burundi lilitoa taarifa hapo siku ya Jumamosi likiwataka wapinzani na waandamanaji kusimamisha bila masharti yoyote, maandamano yao ambayo yamevuruga maisha ya wananchi. Inaonekana kuwa takwa hilo huenda likawakasirisha zaidi wapinzani wanaopinga hatua ya Rais Pierre Nkurunziza ya kuwania tena kiti cha rais na hivyo kuzidisha mvutano kati yao na askari usalama. Tayari mashirika ya kiraia yameitaja amri hiyo kuwa ni tangazo la vita dhidi ya wananchi wa Burundi. Yamesema hakuna rais wa nchi yoyote ile aliyeweza kushinda vita dhidi ya taifa na kumtaka Rais Nkurunziza alitambue vyema suala hilo.
Licha ya kuwa Burundi imekuwa ikishuhudia vitendo vya ghasia na machafuko kwa miezi kadhaa sasa, lakini machafuko hayo yameongezeka kufuatia uamuzi wa Rais Nkurunziza wa kuwania kwa mara ya tatu mfululizo, nafasi ya urais na uamuzi huo kuungwa mkono na Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Wakati huohuo serikali imeimarisha hatua za usalama na kutumia nguvui za jeshi dhidi ya wapinzani. Kufikia sasa makumi ya watu wameuawa na kujeruhiwa katika ghasia zinazoendelea huko Burundi ambapo Warundi wapatao 50,000 wamekimbilia usalama katika nchi jirani, jambo ambalo limeitia wasiwasi mkubwa jamii ya kimataifa. Siku chache zilizopita nchi 15 wananchama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mara nyingine zilitaka kurudishwa utulivu nchini Burundi ili kuandaa mazingira ya kufanyika uchaguzi huru na wa haki nchini. Wakati huohuo Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki imeandaa kikao huko Dar es Salaam mji mkuu wa Tanzania kwa lengo la kutafuta njia za kutatua mgogoro wa Burundi. Wapinzani wa Burundi wanasema kuwa hatua ya Rais Nkurunziza ya kugombea tena uchaguzi inakinzana wazi na katiba ya nchi hiyo pamoja na makubaliano ya Arusha. Licha ya kuwepo ghasia na machafuko nchini Burundi, lakini uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika kama ilivyopangwa, jambo ambalo wapinzani wanasema hawataruhusu litimie, iwapo Rais Nkurunziza ataendelea kushikilia msimamo wake wa kushiriki kwenye uchaguzi huo kinyume cha sheria na katiba ya nchi.

Previous
Next Post »