Mwandishi Wetu
NIJohn Pombe Joseph Magufuli ambaye amepita kwa kishindo na ‘usimpimie’
kuwa mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM)na
mgombea mwenza, Samia Suluhu Hassan, lakini yaliyojiri katika mchakato
wa kumpata mgombea huyo, hayajawahi kutokea, Ijumaa Wikienda limechimba
na kuchimbua.
Mh.John Pombe Joseph Magufuli akiwashukuru wajumbe baada ya kumteua kuwa mgombea wa CCM.
Sarakasi zilikuwa ni nyingi lakini katika kukiokoa chama kisizame mjini
Dodoma, ilibidi kutumia akili nyingi na nguvu ya ziada kumpata mtu clean
(safi) ambaye ni Magufuli.
Uchunguzi wa kina uliofanywa na gazeti hili umebaini kwamba, tangu uhuru
wa Tanzania (1961) hakujawahi kuwa na mvutano mkubwa, ikiwemo wajumbe
kuonesha upinzani dhahiri mbele ya mwanyekiti wao wakati wa mikutano ya
chama hicho katika kumchagua mgombea achilia mbali idadi kubwa ya
waliojitokeza.
Baadhi ya wapiga kura waliozungumza na gazeti hili walisema, mwaka huu
uchaguzi ndani ya CCM umekuwa mgumu kiasi kwamba, hakuna rekodi yoyote
inayofanana nayo hapo miaka ya nyuma.
Akitoa neno baada ya kuteuliwa.
“Mimi nimekuwepo tangu uhuru, sijawahi kuona ugumu wa uchaguzi ndani ya
chama, tangu Tanu (Tanganyika African National Union) mpaka sasa CCM.
Hii ni hali ya hatari.“Kwanza hata wajumbe wenyewe walikosa adabu hata
kwa mwenyekiti wao,” alisema mzee Bakar Masoud, mkazi wa Msasani, Dar.
“Watu wanabebana bwana! Mimi sijawahi kuona, safari hii sijui haya mambo
yametokea wapi?” alisikika mwanachama mmoja wa chama hicho akisema
kutokea mkoani Dodoma.
AWALI, UTARATIBU ULIVYOKUWA
Katika ratiba iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye,
Julai 9, 2015, Kamati Kuu ya CCM (CC) inakaa kupitia majina yote ya
wanachama 38 waliojitokeza kugombea na kuyakata ili kubakisha majina
matano yenye sifa kwa mujibu wa mtazamo wa kamati hiyo.
Yalipatikana majina hayo ambayo ni January Yusuf Makamba, Bernard
Camillus Membe, Asha–Rose Mtengeti Migiro na Balozi Amina Salum
Ali.Julai 10, 2015, Halmashauri Kuu ya CCM (Nec) kukaa kwa lengo la
kupokea hayo majina matano kutoka CC na kuyapigia kura ili yapatikane
majina matatu.
Majina matatu yalipatikana ambayo ni John Magufuli (kura 2104 sawa na
87.1%), Asha-Rose Migiro (kura 59 sawa na 2.4%) na Amina Salum Ali (kura
253 sawa na 10.5%).
Akiwa na mgombea mwenza, Samia Suluhu Hassan.
Julai 11, 2015, Mkutano Mkuu wa CCM kukaa kwa ajili ya kuyapigia kura
majina matatu ili kupata jina moja kwa ajili ya kupeperusha bendera ya
chama hicho dhidi ya wagombea wa upinzani kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa
urais utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
RATIBA YAPANGUKA
Hata hivyo, katika hali isiyokuwa ya kawaida, ratiba zote hizo
hazikwenda sawa baada ya kutokea kwa ugumu uliokuwa nje ya uwezo wa
chama. Hadi Julai 11 siku ya Mkutano Mkuu, Nec walikuwa hawajamaliza
kikao chao hivyo kuingilia ratiba ambayo si yake.
Matokeo yake, Julai 11 kukawa na vikao viwili, Nec iliyoanza saa nne
asubuhi wakiwa wamelala na kiporo walichopewa na CC waliomaliza kikao
saa saba usiku na Mkutano Mkuu ambao ulianza saa mbili usiku.
Mabadiliko mengine yaliyojitokeza ni baada ya matokeo ya kumpata mgombea
mmoja kushindwa kupatikana hadi jana saa 6:30 usiku ambapo mwenyekiti
wa chama hicho aliahirisha kikao mpaka asubuhi ya saa 4:00 tofauti na
miaka mingine ya uchaguzi ndani ya chama hicho.
UPINZANI DHAHIRI
Katika hali ambayo haikutarajiwa, kwenye mkutano wa Nec, wakati viongozi
wa chama kitaifa wakiingia kwenye Ukumbi wa Dodoma Convention, wajumbe
walisimama na kuimba wimbo wa chama huku sehemu ya kumtaja mwenyekiti
(Jakaya Kikwete) wao walichomekea jina la Lowassa (Edward) ambaye
alikuwa miongoni mwa waliojitokeza kugombea lakini jina lake likakatwa
mapema huku kukiwa na malalamiko kwamba, mgombea huyo alionewa.
“Tuna imaaaniii na Lowaaaassa, oyaa! Oyaa! Oyaaa!” baadhi ya wajumbe walisikika wakiimba hivyo.
Baadhi ya wananchi waliokuwa wakifuatilia runingani mkutano huo walisema
kulitaja jina la Lowassa kwa wakati huo ilhali alishakatwa ni uasi na
upinzani, kwani uwepo wa mwenyekiti ulitaka staha zaidi.
WAJUMBE WA CC KUPINGA
Tukio lingine ambalo lilionesha halijawahi kutokea ni kitendo cha
wajumbe watatu kutoka CC kujitokeza hadharani kupinga uamuzi wa wajumbe
wengine.
Wajumbe hao ni Emmanuel Nchimbi aliyekuwa msemaji wa wenzake, Sophia
Simba na Adam Kimbisa ambao walidai kuwa, katika kikao cha kukata majina
matano, kanuni ya chama ya mgombea anayekubalika na wengi ndiye apite,
haikuzingatiwa.
Hata hivyo, Nchimbi hakumtaja mgombea anayependwa na wengi japokuwa wengi walimsemea kuwa alimaanisha Edward Lowassa.
LOWASSA GUMZO
Licha ya jina la Lowassa kukatwa mapema katika hatua ya kushindwa
kuingia ‘Top 5’, jina lake limeendelea kuwa gumzo kila kona ya nchi,
baadhi ya watu wakimzungumzia kwa namna yoyote ile tofauti na wagombea
wengine.
Kwenye mitandao ya kijamii, ishu ni Lowassa hadi gazeti hili linakwenda mitamboni. Baadhi ya watu walitupia hivi:
“Hivi kweli Lowassa wamemkata?! Jamani, kweli CC ni kiboko. Hivi sasa itakuaje?
“Hivi ni kwa nini Lowassa amekatwa? Si walisema ndiye atapita kwenye
Tano Bora, nini kimetokea? Siasa bwana ni ngumu sana.“Lowassa out! Daa!
Kweli CCM ina wenyewe. Lakini naamini hata waliopita wanaweza, mfano
Magufuli, anakubalika pia.”
Kwa upande wake Kikwete alisema kuwa kazi aliyopewa na chama chake ya
kumpata mgombea anayefaa, ameifanikisha na kinachosubiriwa ni ushindi wa
kishindo dhidi ya wapinzani.