manyaki-1.jpg ...      ...

Kenya Airways yapunguza hasara na kuibua matumaini

Wakuu wa Shirika la ndege la Kenya, Kenya Airways, wanasema shirika hilo limepunguza kwa kiwango kikubwa hasara ambayo shirika hilo limekuwa likipata, na kuibua matumaini kwamba huenda shirika hilo likajikwamua.
Matokeo ya kifedha yaliyotangazwa na Mkurugenzi wa kifedha wa shirika hilo Dick Murianki yanaonesha shirika hilo lilipata hasara ya Sh4.73 bilioni kabla ya kulipa ushuru kipindi cha miezi sita hadi kufikia tarehe 30 Septemba.
Huku ni kuimarika kwa 60% ukilinganisha na hasara Sh11.86 bilioni ambayo shirika hilo lilipata kipindi sawa na hicho mwaka 2015.
Bw Murianki amesema mapato ya jumla ya Kenya Airways yalishuka hadi 54.748 bilioni kati ya Aprili na Septemba mwaka huu kutoka 56.72 bilioni kipindi sawa mwaka uliotangulia.
Hata hivyo, idadi ya abiria waliosafirishwa na shirika hilo iliongezeka 4.2% na kufikia 2.2 milioni. Afrika, abiria waliongezeka 14%.
Afisa mkuu mtendaji wa shirika hilo Mbuvi Ngunze amesema kuna matumaini kwamba shirika hilo litajikwamua.
Shirika hilo ambalo humilikiwa asilimia 28.9 na serikali na asilimia 27 na shirika la Air France KLM limekuwa likipunguza idadi yake ya ndege, kuuza baadhi ya mali isiyo ya muhimu sana kama vile ardhi na kupunguza idadi ya wafanyakazi kupunguza hasara.
Shirika hilo kwa kiwango fulani limeathiriwa na kudorora kwa utalii kutokana na wasiwasi wa kiusalama uliosababishwa na mashambulio ya kundi la al-Shabaab kutoka Somalia.
Katika kipindi cha nusu mwaka ya kwanza mwaka huu, Kenya Airways ilipata Sh1.7 bilioni kutoka kwa mauzo ya mali yake.
Kenya Airways kwa sasa imempata mwenyekiti mpya wa bodi ya wakurugenzi, afisa mkuu mtendaji wa zamani wa kampuni ya Safaricom Michael Joseph.
Mwenyekiti wa awali Bw Dennis Awori alijiuzulu Jumatano.
Bw Joseph ameahidi kufufua shirika hilo.
Bei ya hisa za Kenya Airways imeimarika 68% mwezi huu kutokana na matumaini kwamba hali itaimarika sasa baada ya shirika hilo kupata hasara kubwa kwa miaka minne mtawalia.
"Jambo tutakalolipa kipaumbele kwa sasa ni kufanyia mabadiliko mfumo wa ufadhili wa kifedha na hapo baadaye tunaweza kuanza kutathmini suala la kushirikiana na mwekezaji. Lakini kwa sasa ni mapema mno kuzungumzia hilo," Bw Joseph aliambia shirika la habari la Reuters baada ya kuteuliwa.
Kenya Airways hubeba abiria 12,000 kila siku.
Utathmini wa awali ulikuwa umeashiria kwamba shirika hilo linahitaji kuongezewa mtaji wa Sh 70 bilioni ( dola za Marekani 691 milioni).
Previous
Next Post »