Mke wa mgombea urais wa chama cha Republican Donald Trump, Melania, amesema wanawake wanaomtuhumu mumewe kwa kuwadhalilisha kingono ni wanasema uongo, na kusisitiza kwamba Bw Trump ni "mwanamume mstaarabu".
Amesema hata hivyo kwamba matamshi ambayo Bw Donald Trump aliyatoa kwenye kanda ya video ya mwaka 2005 kuhusu wanawake hayakubalini, ingawa amesema hayaonyeshi mwanamume ambaye yeye amemfahamu.
Mgombea huyo wa chama cha Republican ana makosa ya kushiriki "mazungumzo ya wavulana faraghani" lakini alichochewa na mtangazaji wa runinga Billy Bush, Bi Trump amesema.
Kanda hiyo ya ivdoe iliwafanya viongozi wengi wakuu wa chama cha Republican kuacha kumuunga mkono.
Kwenye video hiyo, Bw Trump anaonekana akimwambua Bw Bush, ambaye alikuwa mtangazaji wa kipindi cha Access Hollywood cha NBC, kwamba anaweza kujilazimisha kimapenzi kwa wanawake kwa sababu yeye ni nyota.
Tangu kutolewa kwa kanda hiyo, wanawake kadha wamejitokeza na kudai Bw Trump alidhalilisha kimapenzi, madai ambayo mgombea huyo amekanusha.
"Najua yeye huwaheshimu wanawake lakini anajitetea kwa sababu yanayosemwa ni uongo," Bi Trump amesema kwenye mahojiano na CNN.
"Namwamini mume wangu," amesema.
"Mume wangu ni mkarimu na mwanamume mstaarabu. Hawezi kufanya hayo."
Amedai kashta hiyo "imepangwa na kuandaliwa ili kumzuia kushinda" na kundi la kampeni la mpinzani wake Hillary Clinton na wanahabari.
"Kwa maelezo waliyopata (wanahabari) hawafanyi uchunguzi zaidi kuhusu wanawake hawa? Hawana maelezo ya kweli," ameongeza.
Akiongea kwa mara ya kwanza tangu madai hayo kutokea, Bi Trump amesema mumewe hajawahi kuwadhalilisha wanawake.
Anasema mara kwa mara wanawake walimwendea mumewe mbele yake wakitaka awape namba yake ya simu kwa njia isiyofaa.
Akiongea kuhusu kanda hiyo ya mwaka 2005 ya Access Hollywood ambay ilitolewa kwa wanahabari siku 10 zilizopita, amesema: "Nilimwambia mume wangu, wajua, lugha uliyoitumia haikufaa. Haikubaliki."
"Na nilishangaa kwa sababu huyo si mwanamume ninayemfahamu."
Bi Trump anaamini Billy Bush, ambaye alifutwa kazi na NBC kuhusu kanda hiyo, ndiye wa kulaumiwa.
Bw Trump, alisema, "alihadaiwa, na kupotoshwa na mtangazaji huyo aseme mambo mabaya".
Zimesalia wiki tatu kabla ya uchaguzi na kura za maoni zinaonesha Bw Trump yuko nyuma mpinzani wake wa Democratic Hillary Clinton katika majimbo muhimu yanayoshindaniwa.