Makamu wa rais aliyefutwa kazi nchini Sudan Kusini Riek Machar, ambaye aliikimbia nchi hiyo mwezi Agosti, ameapa kwamba atarejea nchini humo.
Amesema bado anapendwa na watu wa taifa hilo.
AKiongea kutoka Afrika Kusini, Bw Machar ameambia BBC kwamba kundi lake la waasi bado lina matumaini ya kuingia kwenye mkataba wa amani na Rais Salva Kiir.
Amesema hayo licha ya mapigano makali kutokea mjini Malakal kati ya wanajeshi watiifu kwake na wanajeshi wa Rais Kiir.
Bw Machar, ambaye baada ya kutoroka Sudan Kusini alikimbilia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na baadaye akaenda Khartoum, Sudan Kusini, kwa sasa anapokea matibabu Johannesburg.
Mwezi Julai, walinzi wa Bw Machar na walinzi wa Rais Kiir walipigana mjini Juba na kuanzisha vita vilivyodumu siku kadha na kusababisha vifo vya mamia ya watu.
Watu zaidi ya 100,000 walikimbilia nchi jirani.
Mapigano hayo yalizuka chini ya mwaka mmoja baada ya mkataba wa amani uliokuwa umetiwa saini wa kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa na kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Kuchochea vita
Akiongea na kipindi cha HARDtalk cha BBC, Bw Machar amesema: "Nitarejea Sudan Kusini."
"Kwa sababu Rais Salva Kiir hataki uchaguzi huru na wa haki, ndio maana akatushambulia, alianzisha tena vita.
"Lakini natumai kwamba viongozi wenye busara na hekima kutoka kanda hiyo, na Afrika, na maeneo mengine ya dunia wataanzisha mchakato wa kisiasa ambao utarejesha tena amani, na kufufua mkataba wa amani na kuundwa tena kwa serikali ya mpito wa umoja wa kitaifa."
Bw Machar pia amekanusha madai kwamba alichochea vita na badala yake akasema wanajeshi wake walikuwa wanajilinda dhidi ya mashambulizi kutoka kwa wanajeshi wa serikali.
Maafisa wa Rais Kiir wamewatuhumu wanajeshi wa Bw Machar kwa kuanzisha mashambulio hao.
Pande zote mbili zimetuhumiwa kwa kutekeleza uhalifu wakati wa vita.
Majuzi, shirika la Amnesty International lilipendekeza kuundwe mahakama maalum nchini humo ya kuchunguza waliotekeleza uhalifu wakati wa vita.