Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) inasema ina sababu za kimsingi kuamini kuwa wanajeshi wa Marekani wamefanya matendo ya uhalifu wa kivita na hivyo kuashiria kuwepo uwezekano wa kuwafungulia mashitaka.
Katika ripoti yake ya awali, Mwendesha Mashitaka Mkuu wa ICC, Fatou Bensouda, amesema kuwa kwa uchache kuna visa 61 vilivyorikodiwa, ambapo matukio ya utesaji, ukatili na kuvunja heshima ya watu yanahusika. Ripoti hiyo pia inataja visa vyengine 27 vya watu walioteswa na Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) vingi vyao vikitokea baina ya mwaka 2003 na 2004.
Ripoti hii iliyotolewa Jumatatu (14 Novemba) inahoji kwamba uhalifu unaodaiwa kutendeka haukuwa matukio yaliyojitenga kando, bali ni sehemu ya mbinu zilizothibitishwa na Marekani katika majaribio ya kupata taarifa kutoka kwa mahabusu.
"Kuna ushahidi wa kutosha kuamini kuwa uhalifu huu ulitendeteka katika kuendeleza sera ya kupata taarifa kupitia matumizi ya mbinu za mahojiano zinazojumuisha njia za kikatili au fujo, ambazo zingelisaidia malengo ya Marekani nchini Afghanistan." Bensouda anasema kwenye ripoti hiyo.
Marekani yakanusha