manyaki-1.jpg ...      ...

Obama awataka wakuu wa Republican wajitenge na Trump


Barack Obama kwenye kampeni kwa niaba ya Hillary Clinton eneo la Greensboro, North Carolina. 11 Oct 2016Image copyrigh
Image captionRais Obama amesema Donald Trump hafai kuwa rais Marekani
Rais wa Marekani Barack Obama ametoa wito kwa viongozi wakuu wa chama cha Republican kuondoa rasmi uungaji mkono wao kwa mgombea wa chama hicho Donald Trump.
Akiongea katika mkutano wa kampeni wa kumuunga mkono mgombea wa chama cha Democratic Hillary Clinton, Bw Obama amesema haina maana kukemea matamshi ya kudhalilisha ya Bw Trump kuwahusu wanawake bila kujitenga na mgombea huyo.
Akihutubu Greensboro, North Carolina, Jumanne jioni, Rais Obama alishangaa ni vipi wanasiasa wa Republican bado wanataka Bw Trump awe rais.
"Hali kwamba sasa kuna watu wanaosema: 'Sikubaliani kamwe na hili, napinga hilo kabisa ... lakini bado tunamuidhinisha.' Bado wanafikiri anafaa kuwa rais, hilo kwangu halileti maana," alisema.
Bw Obama alisema matamshi ya Bw Trump kuhusu wanawake hata yanaweza kumfanya akose hata kazi ya dukani.
"Sasa unapata hali ambapo huyu bwana anasema mambo ambayo hakuna anayeweza kuyavumilia hata kama mtu huyo angekuwa akiomba kazi (maduka ya) 7-Eleven," alisema.
Bw Obama alikatizwa mara kadha akitoa hotuba na wapinzani wa Bi Clinton lakini alionekana kutoathirika. Badala yake aliwajibu: "Hii ni demokrasia. Hili ni jambo zuri sana."
Watu hao waliokuwa wakimzomea walitolewa nje na maafisa wa usalama.
Maafisa wengi wakuu wa chama cha Republican, akiwemo spika wa bunge la wawakilishi Paul Ryan ambaye ndiye afisa wa ngazi ya juu zaidi wa chama hicho aliyechaguliwa, wameshutumu matamshi hayo ya Bw Trump ambaye anaonekana akijigamba kuhusu kudhalilishwa kwa wanawake kwenye video.
WanaharakatiImage copyright
Image captionWatu kadha walitatiza hotuba ya Bw Obama
Bw Trump hata hivyo amewashambulia vikali wanasiasa hao na kusema ni wasaliti, na kwamba inakuwa vigumu kupambana nao kuliko hata wanasiasa wa chama cha Democratic.
Amesema kwa sasa minyororo iliyokuwa imemfunga imeondolewa na ataipigania Marekani kwa njia anayoitaka.
Donald TrumpImage copyright
Image captionTrump amesema wanasiasa wa Republican wanamshambulia kutoka "kila upande"
Mhariri wa BBC wa masuala ya Amerika Kaskazini anasema kimsingi kwa sasa Bw Trump ni kama anaendesha kampeni yake kama mgombea huru.
Amedokeza kwamba uhasama uliojitokeza kwa sasa utaendelea hata baada ya uchaguzi.
Kwenye kanda ya video ya mwaka 2005 iliyotolewa Ijumaa, Bw Trump anaonekana akieleza jinsi alivyojaribu kuomba kushiriki ngono na mwanamke aliyeolewa pamoja na pia kutoa matamshi mengine ya kuudhi kuhusu wanawake.
Karibu nusu ya maseneta, magavana na wabunge wote 331 wa Republican wameshutumu matamshi hayo ya video na karibu asilimia 10 wametoa wito kwa Bw Trump kujiondoa, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.
Previous
Next Post »