Lowassa, Wasira, Mwandosya, Makongoro kuchukua fomu leo.
Katibu wa Nec, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.
Leo ndiyo siku ya kwanza ya uchukuaji fomu ndani ya CCM kwa ajili
ya kurithi nafasi ya Rais Jakaya Kikwete ambaye anang’atuka kwa mujibu
wa katiba ya nchi.
Makada watakaochukua fomu hizo leo baada ya kutangaza nia kuwania
nafasi hiyo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Mark
Mwandosya; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira; Waziri
Mkuu wa zamani, Edward Lowassa; Balozi wa Umoja wa Afrika (AU) katika
Umoja wa Mataifa (UN), Balozi Amina Salum Ali na Mbunge wa Bunge la
Afrika Mashariki (EALA), Charles Makongoro Nyerere.
Makada hao watatangulia kuchukua fomu hizo huku chama hicho kikitoa masharti makali yanayotakiwa kufuatwa na wagombea.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM wa Idara ya
Oganizesheni, Dk. Mohamed Seif Khatibu, alisema makada watano wataanza
kufungua pazia la uchukuaji fomu leo katika makao makuu CCM mjini
Dodoma.
Alisema katika utaratibu huo, Prof. Mwandosya ndiye atakayekuwa wa kwanza kuchukua fomu saa 4:00 asubuhi akifuatiwa na Wasira.
Dk. Khatibu alisema Lowassa atakuwa wa tatu kuchukua fomu hiyo saa
7:00 mchana, akifuatiwa na Balozi Amina saa 8:30 na Nyerere atafunga
dimba kwa leo.
Alisema ratiba ya uchukuaji fomu hiyo haikupangwa kwa kufuata
umaarufu au cheo cha mtu ndani ya chama na serikali bali umezingatia
mgombea kuwahi kutoa taarifa katika chama kwamba anataka kuchukua fomu.
UCHUKUAJI FOMU Z’BAR
Kwa upande wa Zanzibar, alisema wagombea wanaowania urais wa
Zanzibar watachukulia fomu katika ofisi za CCM na wale wa urais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania watachukulia mjini Dodoma.
“Kama mgombea hawezi kufika Dodoma basi hawezi kuwa Rais, wagombea
wajitokeze kwa muda uliopangwa kuchukua fomu, hatuwezi kukaa hapa
mwezi mzima kuwasubiri wao,” alisema.
YALIYOMO KATIKA FOMU
Alisema fomu zitakazotolewa ambazo zitatakiwa kujazwa zitakuwa na
maelezo binafsi ya mgombea na fomu ya orodha ya wadhamini 450 kama
taratibu, kanuni na sheria zinavyoelekeza.
“Wadhamini wa mgombea hawatakiwi kuwa wajumbe wa mkutano mkuu wa
chama na hawatakiwi kudhamini zaidi ya mgombea mmoja, fomu hizi kabla ya
kuzirejesha zinatakiwa zipigwe mhuri na Katibu wa CCM wa wilaya
anayotoka mgombea,’’ alisema. Aliongeza fomu hizo zitatolewa katika
ofisi ya sekretarieti chini ya usimamizi wake (Khatibu) ambaye amepewa
kazi hiyo na chama.
MASHARTI KWA WAGOMBEA
Alisema kila mgombea atatakiwa kuingia katika ofisi za kuchukulia
fomu akiwa na familia yake ndugu na jamaa wasiozidi 10 na pamoja na Sh.
milioni moja ambazo ni gharama za kuchukulia fomu. Alisema baada ya
kuchukua fomu, kila mgombea atapewa muda wa saa moja na nusu kuwapo
ndani ya jengo la CCM na kuzungumza na waandishi wa habari katika ukumbi
wa Nec na baada ya hapo atatakiwa kuondoka kupisha mwezake.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, Katibu wa Nec, Itikadi na Uenezi, Nape
Nnauye, alisema wakati wa kutoa fomu aliwataka makada hao kuzingatia
kanuni na taratibu za chama ikiwa ni pamoja na kuzisoma ili wasifanye
kinyume cha taratibu na kwamba mbwembwe za aina yoyote haziruhusiwi.
“Tusingependa kuona wale wanaokuja kuchukua fomu na kuzirejesha
wanakuja kwa mbwembwe, hatutaki sherehe wala madoido, safari hii kosa
moja goli moja,” alisema.
Hadi kufikia jana idadi ya makada wa CCM waliotangaza nia ya
kuwania urais hadharani ni Lowassa, Wasira, Mwigulu Nchemba, Prof,
Mwandosya, Nyerere na Balozi Amina, Titus Kamani, Prof. Sospeter
Muhongo, Balozi Ali Abeid Karume, Luhana Mpina na Frederick Sumaye na
Lazaro Nyalandu.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na CCM, kazi ya uchukuaji na
kurejesha fomu itakamika Julai 2, mwaka huu na kufuatiwa na vikao vya
chama vya uteuzi wa kumpata mgombea mmoja atakayepeperusha bendera ya
CCM kupambana na wagombe wa vyama vya upinzani. Mgombea wa CCM
atapatikana Julai 12, mwaka huu baada ya kupitishwa na mkutano mkuu
utakaoanza Julai 11.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imeshatangaza rasmi kuwa uchaguzi
mkuu utafanyika Oktoba 25, mwaka huu kwa ajili ya kuchagua Rais, wabunge
na madiwani.
Wakati huo huo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu
Jumamosi ijayo atahutubia wananchi rasmi akiwa mkoani Singida kabla ya
kuelekea Dodoma kuchukuwa fomu ya kuwania urais.
Nyalandu ambaye amekuwa Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini kwa
miaka kumi sasa, pia atatumia mkutano huo wa hadhara utakaorushwa hewani
moja kwa moja na vituo vya televisheni vya EATV, STAR TV na ITV
kusikiliza hoja mbalimbali kutoka kwa wananchi pamoja na kujibu
maswali yao mbalimbali.
Nyalandu alishatangaza nia ya kuwania urais mapema mwaka huu jimboni kwake mkoani Singida