China imerusha roketi ambayo inawabeba wana anga wawili ambao wataenda kwenye kituo chake cha anga za juu kinachozunguka kwenye mzingo wa dunia.
Wana anga hao waliondoka kutoka chumba cha kurushia roketi na satelaiti cha Jiuquan kaskazini mwa Uchina.
Watatua katika kituo cha anga za juu cha Tiangong 2 ambapo watakaa siku 30, hicho kikiwa kipindi kirefu zaidi ambacho wana anga wa China wamekaa katika anga za juu.
- Mpango wa Marekani kupeleka watu Mars
- Mpango wa kupeleka watu wakaishi Mars
- Mwezi wa Jupiter 'unatoa michirizi ya maji'
Uzinduzi huo na miradi mingine iliyozinduliwa awali ni ishara za kujiandaa kwao kutuma watu Mwezini au katika sayari ya Mars.
Kituo cha awali cha anga za juu kilichoitwa Tiangong, Kasri la Mbinguni, kilifungwa mapema mwaka huu baada ya kupokea roketi tatu.
Wana anga walio kwenye roketi iliyorushwa sasa ni Jing Haipeng, 49, ambaye amewahi kwenda anga za juu awali mara mbili, na Chen Dong, 37.
Roketi hiyo ya Long March-2F imebeba chombo cha anga za juu kilichopewa jina Shenzhou-11, na ilipaa mwendo wa saa 23:30 GMT Jumatatu.
Wana anga hao watakaa kwa muda wakifanya utafiti kwenye kituo cha Tiangong 2.
Rais Xi Jinping akiwapongeza wana anga hao, amesema anatumai ufanisi huo "utaendeleza sana moyo wa usafiri wa anga za juu".
China imewekeza sana katika safari za anga za juu na inapanga kurusha roketi karibu 20 mwaka huu.
China ndiyo nchi ya tatu, baada ya Urusi na Marekani, kutuma binadamu anga za juu kwa kutumia watu kwa kutumia roketi zake binafsi.
China ilizuiwa kutumia Kituo cha Kimataifa cha Anga za Juu (ISS) kutokana na dhana kwamba mpango wake wa anga za juu pia unakusudia kujiimarisha kijeshi