Tanzania na Rwanda zimepiga marufuku uingizaji, usambazaji na utumiaji wa simu za Samsung aina ya Galaxy Note 7.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya visa vya simu hizo kulipuka na kushika moto kuripotiwa nchi mbalimbali, jambo lililoifanya kampuni hiyo kutangaza haitaunda tena simu hizo.
Aidha, Samsung iliwashauri wote waliokuwa wamenunua simu hizo kuzizima na kutozitumia tena.
Nchi hizo mbili za Afrika Mashariki zimefikia uamuzi huo katikati ya wiki iliyopita huku nchi nyingine kama Kenya zikisema hatua ambazo kampuni ya Samsung imezichukua hadi sasa zinatosha.
Kwa mujibu wa gazeti la The East African, Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano TanzaniaBw Innocent Mungy, amewataka wananchi wote ambao wamenunua simu hizo kuzizima na kuzirudisha katika maduka waliyonunulia na wauzaji hao kufuata masharti ya usalama yaliyowekwa na kampuni ya Samsung
"Tumepiga marufuku uingizwaji na utumiaji wa simu hizo," amesema Bw Mungy.
Mashirika mengi ya ndege barani Australia, Ulaya, Asia na Marekani yamepiga marufuku wasafiri kuwa na simu hizo wakati wa safari.
Samsung lilitangaza kuzitoa simu hizo sokoni mwezi Septemba baada ya taarifa kuwa baadhi ya simu hizo zilishika moto wakati wa kuchaji. Wateja walipewa simu nyingine lakini baadaye ilibainika kwamba hata hizo mpya zilikuwa zinashika moto.
Ni hapo ambapo kampuni hiyo iliamua kusitisha kabisa uundaji wa Galaxy Note 7.