Afisa wa habari wa ikulu Josh Earnest amepuuzilia mbali madai ya rais huyo mteule kwamba mamilioni ya watu ambao hawakufaa kupiga kura walishiriki katika uchaguzi huo.
Bw Trump alikuwa pia amedai kwamba kulitokea wizi wa kura katika majimbo ya Virginia, New Hampshire na California, majimbo ambayo Hillary Clinton alishinda.
"Ninachosema ni ukweli mtupu, kwamba hakuna ushahidi wa kuthibitisha madai kama hayo," Bw Earnest aliambia wanahabari White House.
Bw Trump, aliyeshinda uchaguzi kwa kupata kura nyingi za wajumbe, alikuwa amelalamika kuhusu uchaguzi huo kupitia Twitter Jumapili.
"Licha ya kushinda Kura za Wajumbe pakubwa, pia nilishinda kura za kawaida ukiondoa kura za watu ambao hawakufaa kupiga kura lakini walipiga."
Kwenye ujumbe wa kufuatiliza, aliandika: "Ingekuwa rahisi zaidi kwangu kushinda kura za kawaida kuliko Kura za Wajumbe kwa sababu ningehitajika kufanya kampeni katika majimbo 3 au 4 badala ya majimbo 15 ambayo nilitembelea.
"Ningeshinda kwa urahisi hata zaidi na kwa njia ya kuridhisha (lakini majimbo madogo yanasahaulika)!"
- Trump: Mamilioni wasiofaa kupiga kura walipiga
- Wasifu wa Trump, mshindi wa urais Marekani
- Trump alipa dola milioni 25 kumaliza kesi
Rais huyo mteule alianza kulalamika baada ya maafisa wa kampeni wa Clinton kusema wataunga mkono mchakato wa kuhesabiwa upya kwa kura katika jimbo la Wisconsin ambao ulianzishwa na mgombea wa chama cha Green Party Jill Stein.
Bi Stein pia ameifahamisha bodi ya uchaguzi katika jimbo la Michigan, ambapo ushindi wa Bw Trump wa kura 16 za wajumbe ulithibitishwa Jumatatu, kwamba ataomba kura za urais zihesabiwe upya.
Anapanga kufanya jambo sawa jimbo la Pennsylvania.
Bw Trump alishinda kwa kura chache zaidi jimbo la Michigan katika kipindi cha miaka 75 na ndiye mgombea wa kwanza wa Republican kushinda katika jimbo hilo tangu 1988.
Juhudi za Bi Stein za kupigania kuhesabiwa upya kwa kura zinasaidiwa na kampeni ya mitandao ya kijamii ya #recount2016 ambao imesaidia kuchangishwa kwa jumla ya $6.3m (£5m).
Wakati wa kampeni, alifanikiwa tu kuchangisha, $3.5m.
Ili kubadili matokeo ya uchaguzi, itahitaji matokeo yabatilishwe katika majimbo ya Wisconsin, Michigan na Pennsylvania, jambo ambalo wachanganuzi wanasema ni ngumu mno.
Maafisa wa kampeni wa Bi Clinton walisema watashiriki shughuli ya kuhesabu upya kura jimbo la Wisconsin.
Mshauri mkuu wa kampeni Marc Elias alisema hakuna ushahidi kwamba uchaguzi huo uliingiliwa, lakini "tuna wajibu kwa Wamarekani 64 milioni waliompigia kura Hillary Clinton kushiriki katika shughuli hii inayoendelea kuhakikisha matokeo yanayripotiwa ni sahihi."
Jill Stein, 66, ni daktari na mwanaharakati ambaye alitarajia kupata uungwaji mkono kutoka kwa wafuasi wa Democratic waliomuunga mkono Bernie Sanders ambao walikuwa bado wanampinga Bi Clinton uchaguzini.