Rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila siku ya Alhamisi alimteua mbunge wa upinzani, Badibanga Ntita Samy, kama waziri mkuu mpya, ambaye ataongoza serikali ya umoja wa kitaifa hadi pale uchaguzi ulioahirishwa utakapofanyika.
Badibanga Ntita Samy
Uchaguzi uliopangwa kufanyika mwezi huu umeahirishwa hadi Aprili 2018. Serikali iliokuwepo ilijiuzulu mapema wiki hii kufuatana na mkataba kati ya rais na upinzani, unaoruhusu Kabila kubaki madarakani kupita muda rasmi wa muhula wake wa Disemba 19 mwaka huu.
Uteuzi wa Samy kama waziri mkuu umewashangaza wengi kwa kuwa Vital Kamerhe alieongoza upinzani kwenye mazungumzo ya mkataba huo alitarajiwa kuteuliwa kuiongoza serikali hiyo ya mpito.
Kundi lingine la upinzani maarufu kama Rassemblement limepinga mkataba huo likiomba Kabila kuondoka madarakani muda wake ukifika kulingana na katiba. Wanachama wa Ressemblement wanadai kuwa Rais Kabila huenda akatumia muda uliongezwa kubadilisha katiba itakayo toa nafasi kwake kuhudumu kwa muhula mwingine.