Mbunge wa Jimbo la Mikumi ambaye pia ni msanii wa Bongofleva Joseph Haule a.k.a Professor Jay bado anaendelea na harakati zake za kutumikia wananchi wake wa Jimbo la Mikumi kama alivyowaahidi katika kampeni zake za ubunge.
Baada ya kuangahikia tatizo la maji jimboni kwake na kuhakikisha studio yake ya Mwanalizombe inahamia Mikumikwa ajili ya vipaji vya muziki vya jimboni humo, amegeukia upande wa soka na kuamua kuanzisha Ligi ambayo ameiita Professor Jay Cup.
Ligi hiyo ambayo itashirikisha timu 32 kutoka katika kata 15 zaMikumi na kata za jirani, tayari Professor Jay ameanza kwa kukabidhi jezi, mipira na soksi kwa timu zote 32 zilizoomba kushiriki, Ligi itachezwa kwa mfumo wa nyumbani na ugenini na itaanza kwa weekend hii kuchezwa mchezo wa Ngao ya Hisani.