Ripoti iliyoandaliwa kwa hisani ya
umoja wa mataifa imeelezea kuwa oparesheni za kulinda usalama za shirika
hilo zinahitaji kufanyiwa mabadiliko makubwa.
Ripoti hiyo
imekusanywa baada ya madai kutolewa hivi karibuni dhidi ya vikosi vya
umoja huo vya kulinda amani kwamba baadhi wamekuwa wakiwanyanyasa
kingono watoto wadogo.Miongoni mwa mapendekezo ya ripoti hiyo ni kuwa nchi ambako maafisa husika wanatoka, zisikubaliwe kuchangia tena wanajeshi katika vikosi vya umoja wa mataifa.
Pia ripoti hiyo inasema kuwa wanajeshi waliotajwa kuhusika na uovu huo wanastahili wakabiliwe na sheria, na nchi zao pia zinafaa kushurutishwa kueleza wazi ni hatua zipi za adhabu zilizochukuliwa dhidi yao.
Pendekezo jingine lililotolewa katika ripoti hiyo ni kuwa madai yote ya unyanyasaji wa ngono yanastahili kufanyiwa uchunguzi wa kina kwa chini ya miezi sita.